Site icon Bongo Plus

Nyota wa mpira wa kikapu kutoka Tanzania, Hasheem Thabeet (@hasheemthedream) ameandikwa rasmi katika historia ya Chuo Kikuu cha Connecticut kilichopo Storrs Nchini Marekani (UConn) baada ya kuingizwa kwenye ubao wa heshima ya “Huskies of Honor” tarehe 14 Februari, 2026.

Heshima hiyo hutolewa kwa Wachezaji, Makocha na Timu zilizotoa mchango mkubwa na wa kipekee katika historia ya michezo ya Chuo hicho ambapo Majina ya wanaochaguliwa hubandikwa kwenye kuta za ukumbi wa michezo wa Gampel Pavilion ikiwa ni ishara ya kutambua mafanikio yao ya kudumu.

Kwa kawaida ili Mchezaji achaguliwe kuingia kwenye “Huskies of Honor” huwa anatakiwa kuwa amewahi kuchaguliwa kama All-American wa Timu ya kwanza na pia awe amehitimu masomo yake Chuoni hapo ambapo Hasheem Thabeet amekidhi vigezo hivyo huku akikumbukwa kuwa mmoja wa Wachezaji bora waliowahi kuitumikia UConn.

Akiwa na urefu wa futi 7 na inchi 3. Thabeet aliweka rekodi kadhaa za kujivunia Chuoni hapo hususan katika kupiga ‘blocks’ na aliisaidia Timu yake kufikia mafanikio makubwa katika mashindano ya kitaifa mafanikio ambayo yaliweka msingi wa safari yake hadi kufika Ligi ya NBA.

Kuingizwa kwake kwenye “Huskies of Honor” ni ishara ya heshima ya juu kabisa inayotolewa na UConn ukiachia ile ya kustaafishwa kwa namba ya jezi ambapo heshima hii ni fahari si tu kwa UConn bali pia kwa Tanzania ambako Thabeet anabaki kuwa mmoja wa Wachezaji wa kwanza Afrika Mashariki kufikia mafanikio makubwa katika mpira wa kikapu wa kimataifa.

Exit mobile version