Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kutekeleza miradi mipya ya uzalishaji wa umeme badala ya kutegemea vyanzo vya zamani ili kuendana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 08 Februari, 2024 Jijini Dodoma baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Mkataba huo umesainiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kampuni ya Dongfang Electric International kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
“Lazima tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka, mahitaji ya umeme yameongezeka sana lakini vyanzo ni vilevile kwa miaka mingi mfano Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1980, Kidatu mwaka 1975, Kihansi mwaka 2000, Pangani 1995, Hale 1968, Nyumba ya Mungu 1964 na mwaka 2019 baada ya Gesi kuanza uzalishaji umeme mahitaji yalikuwa pungufu kuliko uzalishaji, lakini sasa mahitaji ni makubwa kuliko vyanzo.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko vyanzo vyake, Serikali inaendelea kuongeza vyanzo vipya ikiwemo mradi wa Malagarasi ambao utekelezaji wake utachukua miezi 42 na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajia kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa mwezi huu.
Ameeleza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo mipya ni maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa vyanzo vyote vilivyopo vianze kujengwa sasa ukiwemo miradi ya umeme ya Kakono, Kikonge, Luhudji, Rumakali na miradi ya Gesi mkoani Mtwara ili kuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji ya nchi.
Ili kuwa na umeme kutoka vyanzo mchanganyiko, Dkt, Biteko ametanabaisha kuwa, ameshatoa maagizo kwa watendaji wa Wizara na TANESCO kuhakikisha wanabadilika na kuboresha huduma zao kwa wananchi na kuwezesha uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya Jua na Upepo.
Nchi yetu inakua kwa kasi kubwa, viwanda vingi na migodi mingi inajengwa ambayo inahitaji umeme lakini vyanzo vimebaki kuwa vilevile kutoka mwaka 2016, ndio maana Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tuongeze kasi ili kuwa na chanzo kitakachotupa umeme mwingi zaidi na vingine vyote tuviangalie. Nafurahi kuwaeleza kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere umefikia asilimia 96 na hii ina maana kuwa tuko tayari na mwezi huu wa Pili tutaingiza umeme wa JNHPP kwenye gridi ya Taifa.” Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko. Tarehe 08 Februari 2024.
