Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeteketeza kilogramu 614.12 za dawa za kulevya katika kiwanda kimoja cha saruji eneo la Wazo, Dar es salaam.
Akiongea na Waandishi wa Habari katika eneo hilo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema kati ya dawa zilizoteketezwa, kilogramu 601.87 ni
methamphetamine na kilogramu 12.25 ni heroin ambapo dawa hizo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo
Mahakama za Hakimu Mkazi Kibaha na Kisutu ziliamuru uteketezaji wake kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo wakati kesi husika bado zinaendelea.
“Uteketezaji wa dawa hizi unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake, sheria hii inaruhusu uteketezaji wa dawa hizi kufanyika kabla, wakati, au baada ya shauri kumalizika Mahakaamani”
Kamishna amesema uteketezaji huo unafanywa kwa njia zinazozingatia usalama wa afya ya Watu na utunzaji wa mazingira huku ukisimamiwa na Wadau mbalimbali
waliotajwa kisheria.
Kamishna Lyimo amesema kuwa katika mwezi huu wa December pekee, Mamlaka imefanikiwa kuteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika Mkoa wa Tabora,
pamoja na kilogramu 398.105 za dawa mbalimbali mkoani Mtwara, pia Mamlaka inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi Mkoani Arusha katika siku chache zijazo.

