Mwanafunzi wa Chuo cha Utalii Marangu, mkoani Kilimanjaro, Clara Kimathi (21) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na ‘house boy’ wa familia aliyokuwa akiishi kwa madai ya kukataa kumpa penzi.
Mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na moja ya familia iliyopo kitongoji cha Mieresini, Kata ya Makuyuni Wilaya ya Moshi baada ya baba na mama yake kufariki dunia miaka michache iliyopita.
Inaelezwa kuwa baada ya mwanafunzi huyo kujeruhiwa Desemba 5 mwaka jana, alikuwa amelazwa Hospitali ya KCMC kwa zaidi ya miezi miwili ambapo hali yake haikutengamaa kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata, ambapo inadaiwa alichomwa visu vitano vya tumboni, mgongoni na kusababisha utumbo kutoka nje na ilipofika Februari 25, mvwaka huu alifariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi digital leo Machi Mosi, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Desemba 5, mwaka jana na tayari hatua kadhaa za kisheria zilishachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.