Benki ya CRDB Bank Plc imetangaza kuendelea kuimarika kifedha baada ya kurekodi ongezeko la faida katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 18.9 na kufikia shilingi bilioni 206.2, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Aidha, jumla ya mali za benki hiyo zimeongezeka kwa asilimia 7.1 hadi kufikia shilingi trilioni 23.9, huku mikopo kwa wateja ikiongezeka kwa asilimia 6.8 hadi trilioni 14.7. Amana za wateja nazo zimekua kwa asilimia tisa na kufikia trilioni 16.2.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema ukuaji huo unatokana na utekelezaji thabiti wa mkakati wa biashara unaolenga kutoa thamani kwa wateja, kukuza uchumi, na kuongeza manufaa kwa wanahisa.

