Klabu ya Simba iko mbioni kuachana na kocha wa makipa, Mhispania Dani Cadena 🇪🇸 wakati mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeiambia Arena kwamba, Cadena hana mpango wa kuongeza mkataba ingawa viongozi wa Simba wanapambana kumuongezea mwaka mmoja zaidi, lakini matatizo ya kifamilia yanamuondoa.
.
Alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba kukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine ila yeye mwenyewe ameonyesha kwamba hayupo tayari kuendelea nasi kwa msimu ujao japo viongozi wanapambana kwa ajili ya kumbakisha. “Anasema ana matatizo ya kifamilia na anataka kukaa karibu na familia yake kwa sasa,” kilisema chanzo.
.
Cadena alipotafutwa alisema kwa sasa nguvu na akili ameviwekeza kumalizia michezo ya Ligi Kuu iliyobaki na baada ya hapo ndipo ataweka wazi juu ya hatima yake ndani ya kikosi hicho. Licha ya kauli hiyo, lakini mtu wake wa karibu amesema kwamba kocha huyo hayupo tayari kubaki Tanzania huku sababu kubwa ikielezwa ni kutokana na umbali alionao na familia yake yenye makazi nchini Hispania.

