Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali maombi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu kujitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Lissu anayewakilishwa na Jopo la Mawakili zaidi ya 30, aliwasilisha maombi hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franko Kiswaga baada ya Jopo la Mawakili wanaomtetea kujitambulisha.
Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Hakimu Kiswaga alisema anakubaliana na maombi hayo hivyo Lissu atajitetea mwenyewe hadi pale atakaposema basi.
“Kwahiyo kuanzia sasa hoja zitakuwa zinajibiwa kutoka kwa Upande wa Serikali dhidi ya mshtakiwa. Mahakama imemkubalia ombi la kujitetea hadi atakaposema basi,”
“Pia mnapokuwa mahakamani maafisa usalama msizuie mshtakiwa kupewa nyaraka na Mawakili wake,”.
Pia Hakimu Kiswaga aliutaka Upande wa Serikali kujibu hoja hizo, ambapo Wakili Nassoro Katuga alisema hawana pingamizi na mshtakiwa kujitetea mwenyewe, pia kuhusu hoja za gerezani zinapaswa kujibiwa na Magereza wenyewe.
