Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Dar es Salaam imetoa amri ya kutotajwa majina ya mashahidi wala maelezo yao yanayoweza kuwatambulisha katika kesi ya mauaji ya askari polisi wawili.
Askari polisi E.177 Koplo Michael na D.2865 Sajini Francis waliuawa kwa kupigwa risasi Aprili 2015 na kuporwa silaha katika tukio lililotokea Mkoa wa Kipolisi Temeke, Dar es Salaam linalohusishwa na matendo ya kigaidi.
Kutokana na sababu za kiusalama, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) aliwasilisha ombi la kusikilizwa upande mmoja akiiomba Mahakama itoe amri kuzuia
kutaja utambulisho wa mashahidi na mahali walipo.
Maombi hayo namba 26910 dhidi ya Hassan Kube (mshitakiwa wa kwanza) na Mohamed Hassan (mshitakiwa wa pili) yalisikilizwa Desemba 13, 2024 na Jaji Mfawidhi Awamu Mbagwa.
DPP aliomba Mahakama itoe zuio hilo wakati kesi ya mauaji namba 2 ya mwaka 2023 itakopopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Pia, aliomba kutowekwa wazi maelezo na nyaraka zinazoweza kuwatambulisha mashahidi wakati wa usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili wa kesi hiyo ya jinai.

