Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda leo, Jumapili Aprili 28.2024 amekutana kwa ajili ya mazungumzo na kikundi cha vijana wanaojihusha na mchezo wa kuendesha Pikipiki Arusha ambapo amewapongeza kwa kazi wanayoifanya hata hivyo ametoa wito kwa vijana hao kuendelea kuamini katika ndoto zao, na kwamba kupitia mchezo huo wanapaswa kutimiza ndoto hizo
Katika kuhakikisha ndoto za vijana hao zinatimia Makonda amewataka kuunda uongozi haraka iwezekanavyo, ambapo pamoja na mambo mengine uongozi huo utashirikiana na ofisi yake (ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha) katika kuandaa mipango ya kuhakikisha mchezo huo unatangazwa kama sehemu ya kivutio cha Arusha, hiyo ikienda sambamba na wachezaji wake kunufaika kwa kujipatia kipato kitakachoweza kuendesha maisha yao kama ilivyo kwa wanamichezo wengine
Amesema miongoni mwa mambo anayokusudia kufanya ni pamoja na kuandaa mashindano maalumu ambayo licha ya kwamba mashindano hayo yatatafutiwa wadhamini lakini ofisi yake kwanza inakusudia kutoa zawadi ya shilingi milioni 10 kwa mshidi wa kwanza, milioni saba (7) kwa aliyeshika nafasi ya pili na shilingi milioni tano (5) kwa mtu wa tatu, kiasi ambacho kinaweza kuongezeka kutokana na idadi ya wadhamini watakojitokeza na kiasi cha pesa watakachotoa
Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya vijana hao wamemuomba Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuhakikisha anawatafutia kiwanja eneo maalumu watakalokuwa wanalitumia kwa ajili ya mazoezi kwa kuwa miongoni mwa changamoto inayowakabili kwa sasa ni kukosa eneo la kufanyia mchezo huo
Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye viunga vya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, vijana hao pia wamemuonesha Makonda umahiri wao wa kucheza mchezo huo wa kuendesha Pikipiki jambo ambalo liliibua hisia mseto kutoka kwa watazamaji waliokuwa kwenye eneo hilo

