Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni maalum mkoani Morogoro kwa muda wa siku tisa katika vijiji vya Nyarutanga, Lujenge na Mafumbo vilivyopo wilaya za Morogoro vijijini na Kilosa.
Katika vijiji vya mafumbo na Lujenge Mamlaka imeteketeza jumla ya ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi.
Aidha, katika operesheni iliyofanyika kijiji cha Nyarutanga watu 6 wakiwa na kilogramu 342 za bangi wamekamatwa na watafikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Akizungumza mara baada ya utekelezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa mto Mbakana, Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.

