Site icon Bongo Plus

Mhe. Dkt. Doto Biteko ameelezaanataka kuona viongozi wote wanatatua kero na changamoto za wananchi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona viongozi wote wanatatua kero na changamoto za wananchi na kwamba anasikitishwa na baadhi ya viongozi ambao hawatatui changamoto za wananchi mpaka pale anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 25 Januari, 2024 wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga mkoani Tanga mara baada ya kuwasha umeme katika vijiji hivyo ambao umesambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“Mhe. Rais anafanya kazi kubwa katika kila Sekta na mabilioni ya pesa yamekuwa yakipelekwa kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi, nikitolea mfano hapa Tanga Serikali ya Awamu ya Sita imeshaleta shilingi Trilioni 2 na Bilioni 600 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kwenye umeme miradi inaongezeka kwani mmepata bilioni 133.6 huku Wilaya ya Mkinga ikipata bilioni Nane kwa ajili ya usambazaji umeme, Dkt. Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora watanzania hivyo viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu bali tuzitatue na kama kuna mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi.” Amesema Dkt.Biteko

Kuhusu usambazaji umeme vijijini, amepongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme vijijini akitolea mfano kuwa, usambazaji umeme vijijini mkoani Tanga umefanyika kwa asilimia 91 na wilaya ya Mkinga yenye Vijiji 85 tayari vijiji 82 vimesambaziwa umeme huku kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyosalia ikiendelea na baadaye vitafuata vitongoji.

Kuhusu hali ya umeme nchini, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya kila jitihada kuboresha hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa mitambo ya umeme inafanyiwa maboresho na miradi mipya inaanzishwa na kutekelezwa akitolea mfano kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) kinatarajiwa kuzalisha umeme baada ya siku mbili baada ya kufanyiwa maboresho.

Exit mobile version