Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila leo June 30,2025 amemuapisha Mkuu wa Wilaya mpya wa Kigamboni Dalmia Mikaya (Dalmiamikaya) ambapo DC Dalmia ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kutatua changamoto za Wananchi wa Kigamboni.
Akiongea baada ya kula kiapo Jijini Dar es salaam leo, DC Dalmia amesema “Namshukuru Mungu kwa siku ya leo ya kipekee, namshukuru sana kwa dhati ya moyo wangu Rais wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunipa fursa ya kunipandisha hadhi kutoka kuwa Katibu Tawala wa Wilaya hadi kuwa Mkuu wa Wilaya, ni nafasi ya kipekee nami niahidi kuchapa kazi na pia kushirikina na Viongozi wenzangu wa Chama na Serikali”
“Natambua Wananchi wetu wa Kigamboni wana matarajio ya sisi kuwajibika na kufanya kazi na kuwatumikia nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunasimamia shughuli za Serikali kwa kusikiliza na kutatua changamoto za Wananchi, kukusanya mapato, kusimamia usafi na shughuli nyingine za msingi”
“Natambua wapo Wakuu wa Wilaya wenzangu hapa ukumbini, naahidi nitakupa ushirikiano kwa asilimia 100 Mh. Mkuu wa Mkoa(Albert Chalamila) na kushirikiana na Wakuu wa Wilaya wenzangu ili kukusaidia Mkuu wa Mkoa ili kuziletea maendeleo Wilaya zetu”
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Dalmia kuwa DC mpya wa Kigamboni hivi karibuni akitokea kwenye nafasi ya Ukatibu Tawala (DAS) Wilaya ya Tanga na anachukua nafasi ya Halima Bulembo ambaye anaenda kugombea Ubunge
