Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, amewataka wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Mazingira kuchangamkia fursa ya Maonesho Makubwa ya Kilimo Biashara yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Gairo kuanzia Oktoba 06, 2024 hadi Oktoba 12, 2024.
Rai hiyo ameitoa Leo wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia Maonesho hayo ambayo yatawaleta pamoja wadau wote wanaohusika katika Mnyororo wa Thamani wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Mazingira wakiwemo Wakulima na Wafugaji , Wauzaji na Wazalishaji wa Pembejeo za Kilimo na Mifugo, Taasisi za Fedha, Taasisi za Utafiti katika Sekta ya Kilimo na Mifugo, Wasindikaji na Wafanyabiashara, Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na Shughuli za Kilimo, Mifugo na Mazingira, Taasisi za Umma na Binafsi zinazotoa Huduma ambatano kwa wakulima na wafugaji ikiwemo Taasisi za Bima, Hifadhi ya Jamii, Nishati Safi ya Kupikia, nk
Aidha, Mhe. Malima amewataka wakulima na wafugaji kuchangamkia fursa hiyo kwenda kujifunza mbinu na Teknolojia Bora na za kisasa za Ufugaji na Kilimo Bora ili iwasaidie katika kupambana na umasikini, kwani Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania amewekeza vya kutosha katika Kilimo na Mifugo ili kuzifanya Sekta hizo kukua na kuwakomboa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabiri Makame alisema zaidi ya asilimia 95 ya Wananchi wa Gairo wanajishughulisha katika Sekta ya Kilimo na Mifugo hivyo Sekta hizi ndiyo muhimili wa kukuza Pato la Mwananchi mmoja mmoja, kukuza uchumi wa Wilaya na Kuongeza Ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri.
