Mzozo wa kifamilia uliowahi kuivunja P-Square, moja ya makundi bora zaidi Afrika umerudi tena kwenye mitandao ya kijamii baada ya kaka mkubwa wa Peter na Paul, ambaye pia alikuwa meneja wao wa zamani, Jude Okoye, kuchapisha ujumbe tata kwenye Instagram.
Ingawa hakumtaja mtu moja kwa moja, Jude alidai kuwa aliwainua watu waliogeuka na kuwa wasaliti waliojawa na tamaa, wakamsingizia tuhuma za utakatishaji fedha na kutaka kumlazimisha awape pesa. Haya maneno yalionekana kumlenga Peter Okoye (Mr. P), ambaye hakusita kujibu.
Katika jibu lake kali, Peter aliweka wazi yafuatayo:
Usimamizi: Alisema Jude hakuwa mkombozi wa kundi hilo bali alikuwa mfanyakazi wao kama mameneja waliomtangulia, na alifutwa kazi baada ya kuonyesha uongozi usioridhisha.
Kufilisika: Alikanusha kuwa amefilisika, akidai ni Jude mwenyewe aliyeeneza simulizi hiyo kwa chuki ya muda mrefu.
Heshima: Alimtaja Jude kama “Agbaya” neno la Kiyoruba linalomaanisha mtu mzima mwenye tabia za kitoto akisisitiza kuwa heshima haiji kwa umri bali kwa vitendo.
Tangu miaka ya nyuma, kukosekana kwa uwazi kuhusu fedha, ubunifu na nafasi ya Jude kwenye kundi kulisababisha migogoro ya ndani. Hatimaye, P-Square walisambaratika mwaka 2017, hali iliyosikitisha mashabiki duniani kote.
Lakini katika kile kilichoonekana kama muujiza wa muziki, mwaka 2021, Peter na Paul walipatana na kurudisha kundi lao, hatua iliyopokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa Afropop, lakini waliachana tena na kila mmoja kuendelea na maisha yake.

