Mtoto Asimwe Novarti mwenye ulemavu wa ngozi (albino) aliyeibwa Mei 30 mwaka huu na watu wasiojulikana katika kijiji cha Mbale wilayani Muleba, amekutwa ameuawa na kisha mwili wake kufungwa kwenye sandarusi na kutelekezwa kwenye moja ya kalavati huku baadhi ya viungo vya vyake vikiwa vimenyofolewa.
Katibu Tawala wa wilaya ya Muleba, Benjamin Mwikasyege amesema mwili ulikutwa umefungwa kwenye mfuko kabla kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mtoto Asimwe Novarti aliyekuwa na miaka miwili aliibwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana ambao walifika na kudai wanahitaji msaada kutoka kwa mama wa familia hiyo ambaye baada ya kutoka ndani ili kutoa msaada walimkaba na kisha kutokomea na mtoto huyo.