Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio linalomhusisha mwanafunzi wa kidato cha nne, Julitha Saimon (18) siyo jina lake sahihi, kutoka Shule ya Sekondari Nkasi, ambaye alijifungua na kisha kumtupa mtoto chooni.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Aprili 16, 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija amesema inadaiwa wiki iliyopita, mwanafunzi huyo alijifungua mtoto kisha kumtumbukiza kwenye shimo la choo cha nyumbani kwao na baadaye akaelekea shuleni kuendelea na masomo.
“Lakini asubuhi hiyo, baadhi ya watu waliopita karibu na choo hicho, walisikia sauti ya mtoto huyo ikitoka ndani ya choo wakachukua hatua ya kuja kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, tuliwatuma askari eneo hilo na wakamuokoa mtoto huyo ambaye mpaka sasa yuko hai na anaendelea vizuri,” amesema kamanda huyo.
Amesema baada ya ukoaji huo, mtoto aliwahishwa hospitali kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, amesema baada ya binti huyo kuhojiwa, alikiri kufanya tukio hilo na hajui ni nini kilimsukuma amtupe mwanawe chooni baada ya kujifungua.