Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 1 Aprili, 2024 ametembelea Kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu, wilayani Kilombero mkoani Morogoro kukagua matengenezo ya Mitambo ya umeme kufuatia hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha maji kwenye mitambo hiyo ambayo imesababisha athari kwenye Gridi ya Taifa na kupelekea maeneo mengi ya Nchi kukosa huduma ya umeme.
📌Aigaza TANESCO kutafuta mwarobaini wa tatizo la kufeli kwa Gridi mara kwa mara
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara ya dharura katika Kituo cha kufua umeme cha Kidatu, Mkoani Morogoro kufuatia kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa jana usiku na kusababisha mikoa mingi Tanzania Bara na Zanzibar kukosa huduma ya umeme.
Mhe. Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linatafuta suluhisho la kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa mara kwa mara.
Aidha, amewataka TANESCO kuhakikisha wanafanya upembuzi wa kina ili kuboresha miundombinu kwenye Gridi na kuongeza kuwa matatizo kama hayo yanapojitokeza yawe funzo yasijitokeze tena.
“Nawaomba radhi sana wananchi na watanzania kwa ujumla kufuatia hitilafu hii kwenye mfumo wa Gridi, kwani imeleta usumbufu na changamoto kwa wananchi kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama” alisisitiza Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa vipato vya wananchi vinategemea zaidi uwepo wa nishati ya umeme hivyo TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo wakati wote.
Dkt. Biteko amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo-Hanga kwa kuchukua hatua za haraka kufika kwenye eneo la changamoto bila kusukumwa bali kwa kujiongeza.
Aidha, Dkt Biteko, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, kuhakikisha timu yote ya wataalamu inashirikiana ili kupata suluhu ya changamoto hiyo ya umeme na kuiondoa kabisa.
Pia, amewatahadharisha TANESCO kuchukua tahadhari hususan katika kipindi hiki cha kiwango kikubwa cha mvua zinazonyesha na kuwataka TANESCO kuchukua tahadhari kwani maji yanayoingia kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ni kikubwa na kutolea mfano wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere ili kuondoa madhara yanayoweza kusababishwa na wingi wa maji hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Danstan Kyoba amewashukuru Wizara ya Nishati kwa hatua ilizochukua kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa wakati na kuwatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari kufuatia kiwango kikubwa cha mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kuharibu miundombinu mbalimbali.

