Abiria 257 wa Shirika la Ndege la United Airlines walikumbwa na mshangao baada ya ndege yao kurejea ghafla Marekani, ikiwa safarini kuelekea Shanghai, China kisa mmoja wa marubani alikuwa amesahau pasipoti.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787, iliyokuwa ikitekeleza safari ya UA 198, iliondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Los Angeles (LAX) mnamo Jumamosi, Machi 22, saa 8 mchana. Baada ya takriban saa mbili angani, iligeuza mwelekeo na kutua San Francisco saa 11 jioni, baada ya kugundulika kuwa rubani amesahau pasipoti yake
Kulingana na taarifa ya United Airlines kwa CNN, kampuni hiyo ilisema, “Rubani hakuwa na pasipoti yake ndani ya ndege. Tuliratibu upya safari na kuweka marubani wapya ili kuwasafirisha abiria usiku huo.”
Baada ya kutua San Francisco, abiria walipatiwa vocha za chakula zenye thamani ya dola 30 kila mmoja na fidia nyingine kupitia mfumo wa malalamiko wa shirika hilo.
Aidha, ndege mpya iliondoka San Francisco saa 3 usiku na kutua Shanghai saa 6 baadaye, ikiwa imechelewa kwa takriban saa sita.