
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayowaonyesha watu wawili wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari mfanyabiashara, eneo la Kiluvya jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Jumatano Novemba 13, 2024 imesema kjana aliyekuwa akiingizwa kwa nguvu kwenye gari anafahamika kwa jina la
Deogratius Tarimo.
“Jeshi la Polisi linachunguza picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu ambao wanajaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani
ya gari, Deogratius Tarimo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha, mkoani Pwani. Tukio hili liliripotiwa na yeye mwenyewe katika kituo cha Polisi Gogoni Jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2024,’imesema taarifa hiyo.
Katika video yenye sekunde 49 iliyoanza kusambaa jana Novemba 12, 2024 usiku katika mitandao ya kijamii ilimuonyesha kijana huyo (aliyetambuliwa kama
Deogratius Tarimo) akiwa analazimishwa kuingia ndani ya gari aina ya Toyota Raumu na vijana wawili.

