Rais wa Marekani, Donald Trump, alionyesha mshangao na kuvutiwa na muonekano wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wakati wa mkutano wao uliofanyika Ikulu ya Marekani siku ya Jumatatu.
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na waandishi wa habari na maafisa wa serikali, Trump alimpongeza Zelensky kwa kile alichokiita “suti nzuri na ya kuvutia”. Trump alisikika akisema: “I cannot believe it, I love it,” akielekeza maneno hayo kwa Zelensky aliyekuwa amevalia suti nyeusi rasmi, tofauti na mavazi yake ya kijeshi ya kawaida.
Zelensky, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionekana katika mavazi yasiyo rasmi ya kijeshi tangu uvamizi wa Urusi kuanza, alibadili muonekano wake kwa tukio hilo muhimu la kidiplomasia, jambo lililozua maoni mengi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wachambuzi wa siasa wanasema tukio hilo linaonyesha hatua ya Zelensky kutaka kuimarisha sura ya kidiplomasia ya Ukraine mbele ya Marekani na dunia kwa ujumla, hasa katika nyakati hizi ambapo usaidizi wa kimataifa unaendelea kuhitajika kwa ajili ya taifa lake.
Mkutano huo uliangazia masuala ya msaada wa kijeshi, uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, na mustakabali wa vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi.
