Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza amesema hakuna Taifa linalokosa Watukutu lakini Watukutu hao hawapaswi kupotezwa, kutekwa au kuuawa huku akisema amani haiwezi kupatikana pasipo na haki na wasiopenda haki ndio wanasababisha fujo.
Askofu Nkwande amesema hayo wakati akitoa taarifa Kanisani baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kuthibitisha kumpata Padre Camillius Nikata wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea, ambaye alikuwa ameripotiwa kupotea tangu October 9, 2025 na kupatikana akiwa salama katika mashamba ya Kijiji cha Mawa, Kata ya Hanga Wilayanu Namtumbo.
Askofu Nkwande amesema “Padri aliyepotea ni Padri wa Songea kwa asili lakini anafanya kazi katika Jimbo hili, kwa muda huu ni Padri wa Mwanza, kama alishapanga kuacha Upadri Mimi napaswa kujua, Mimi sijui Askofu wa Songea hajui, Watu wanasema alishaomba hakusikilizwa, Mapdri hivi ukitaka kuacha Upadri unasikilizwa?, si unaondoka
“Badala ya kupata maneno ya kututi moyo tusikate tamaa, tunapewa maneno ya maudhi tunaudhiwa, tunapofungua Parokia zetu hizi tusali tuombe amani, na Viongozi wetu watafute fursa ya kutia moyo na kulifariji Taifa, Taifa limegawanyika, Taifa lina mahangaiko”
“Katika Taifa hauwezi kukosa Watu Watukutu lakini ni Wananchi wa hapa, utukutu wao sio wa kumpoteza wala kumteka au kumuua, leo tunatembea huko hatujiamini, Watanzania tulikuwa tunaheshimika katika Ulimwengu, wapo wanaoniuliza sasa nyie mkiwa hivi tutakimbilia wapi?, hapa tunaanza kufanyiana hivyo sababu ya nini?, tatizo ni nini?”
“Tunahitaji kweli amani lakini tutambue kama tunaitafuta amani lazima iwepo haki, kuitafuta na kuipata amani pasipo haki ni uongo, haki lazima iwepo ili tujue asiyeipenda haki ni nani, huyo ndiye tutakayesema anasababisha fujo, tumuombe Mungu atusaidie Taifa letu liwe la haki ili tuipate amani tuliyokuwa tumeizoea na amani itatufanya tuwe huru”

