Site icon Bongo Plus

TANESCO YAONGEZA MITAMBO MIWILI YA KUZALISHA UMEME MAFI

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeongeza mitambo miwili ya uzalishaji umeme katika kituo kikuu cha umeme wilayani Mafia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia TANESCO za kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika wakati wote.

Mitambo hiyo ina uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati mbili ambapo kila mtambo mmoja utazalisha megawati moja.

Akizungumzia juu ya mitambo hiyo, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mafia Mha. Seif Kijanga amesema,

“Katika Wilaya yetu ya Mafia hivi karibuni tumepokea mashine mbili, mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati mbili tunatarajia baada kukamilika ufungaji wa mitambo hii tutakua na upatikanaji mzuri wa umeme wa uhakika”.

Kwa upande wake Mhandisi Mariam Patrick, ambaye ni mratibu wa mradi alieleza kuwa ujio wa mitambo hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Shirika katika kuboresha huduma kwa wananchi.

“Kupitia mitambo hii, tumeongeza uwezo wa uzalishaji mara mbili zaidi ya awali, jambo litakalopunguza kero za kukatika kwa umeme na kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa Mafia,” amesema Mha. Mariam.

Nao baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Mafia wameonekana kufurahishwa na mradi huo huku wakieleza matumaini yao juu ya hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo.

“Huu mradi utatusaidia sana sisi kama wafanyabiashara wa Wilaya ya Mafia kwa sababu hapo awali kulikua na changamoto ya umeme hivyo tunaimani mradi huu ukikamilika changamoto itakua imeisha” amesema Khamis Ahmed.

Naye Bi. Tabia Kiwambe amesema TANESCO imekua mstari wa mbele katika kutoa huduma bora na anaimani na namna Shirika hilo linafanya kazi.

“Sisi hatuna shida na TANESCO kabisa na umeme ndio kila kitu, kama hakuna umeme hakuna maendeleo” ameongeza Bi. Tabia.

Ufungwaji wa mashine hizo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TANESCO kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa Mafia inaimarika

 

Exit mobile version