Tanzania imesisitiza kuendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa lilanoshughulikia Wahamiaji (IOM) kuwawezesha vijana kiuchumi ili kutengeneza ajira zitakazojenga ustawi wao na kuleta maendeleo kwa taifa.
Msisitizo huo umetolewa leo tarehe 15 Agosti, 2024 wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo alipokutana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wahamiaji (IOM) Bw. Mohammed ABDIKER jijini Harare, Zimbabwe.
Aidha, katika mazungungumzo hayo Waziri Kombo ameeleza changamoto ya uhamiaji huwaathiri zaidi vijana wanaotoka katika mataifa yanayoendelea hususan mataifa ya Afrika ambapo wamekuwa wakihama kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yao na familia zao.
“Binafsi ningependa tatizo la uhamiaji lipate suluhisho kwa kufanyia kazi chanzo cha tatizo badala ya kufanyia kazi matokeo au matatizo yanayotokea baada ya watu kuhama na kupata changamoto wakiwa katika harakati za kuvuka mipaka” alisema Waziri Kombo.

