Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akiwa katika ziara ya kikazi jijini Budapest, amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Veronika Varga-Bajusz, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Uvumbuzi wa Hungary anayesimamia masuala ya elimu ya juu.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo katika sekta ya elimu. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Kombo aliishukuru Serikali ya Hungary kwa utaratibu wake wa kutoa nafasi 30 za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini Hungary.
Aidha, Mhe. Kombo alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo ya ufadhili ili kuwezesha wanafunzi wengi kutoka Tanzania kunufaika na utalaam wa Hungary katika sekta muhimu kama tiba na dawa, uhandisi na kilimo.
Vilevile, viongozi hao wamejadili juu ya Serikali ya Hungary kuanzisha programu ya kubadilishana watalaam ili kushirishana teknolojia na utalaam katika sekta za kipaumbele kama vile, kilimo, afya na tiba, uhandisi hususan uhandisi wa maji.
Naye, Katibu Mkuu Bi. Veronika alieleza kuwa suala hilo litasaidia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana utalaam na kuwawezesha wataalam wa pande mbili kuandaa program za kubadilishana ujuzi na mafunzo ya muda mfupi katika fani za kipaumbele.