Daktari Livin Mumburi ameandika historia mpya nchini baada ya kuwa daktari bingwa wa kwanza wa magonjwa ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kwa watoto, katikati ya changamoto ya magonjwa ya mfumo wa chakula kwa watoto.
Kwa mujibu wa ukurasa wa mtandao wa kijamii wa African Pediatric Fellowship wa Facebook, Dk Mumburi ameandika historia hiyo baada ya kuhitimu kwa mafanikio makubwa ubingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula kwa watoto kupitia Chuo cha Tiba cha Afrika Kusini, hatua inayomuweka miongoni mwa wataalamu wachache barani Afrika katika fani hiyo.
Akiwa anatarajia kurejea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), uwepo wake unatarajiwa kuleta mapinduzi katika huduma za afya kwa watoto.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu, Aprili 20, 2026, kuhusu umuhimu wa utaalamu huo, Dk Mumburi amesema mahitaji ya huduma za kibingwa kwa watoto wenye matatizo ya mfumo wa chakula na ini ni makubwa kuliko ilivyodhaniwa.
“Uhitaji ni mkubwa sana, kwa sababu hata kabla sijaenda kufanya mafunzo ya ubingwa nilikuwa nakutana na watoto wengi wenye changamoto kubwa za mfumo wa chakula na magonjwa ya ini. Hii inaonesha wazi bado tuna pengo kubwa la wataalamu katika eneo hili,” amesema.
Ameongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza idadi ya wataalamu wa fani hiyo nchini.

