Site icon Bongo Plus

Trump Aanza Urais Kwa Kufuta Maagizo Ya Biden

Rais Donald Trump ameanza muhula
wake wa pili kwa kufuta maagizo 78 ya enzi ya Rais Joe Biden, ikiwemo maagizo ya rais, memoranda za urais, na hatua nyingine za kiutawala. Katika siku ya kwanza tu, alisaini jumla ya maagizo zaidi ya 200, yakiwemo maagizo 42 ya rais na hatua 115 za ajira serikalini.

Trump alitangaza kufutwa kwa miongozo hiyo iliyowekwa na utawala uliopita na pia kuweka zuio la muda kwa utekelezaji wa kanuni mpya za shirikisho hadi zitakapopitiwa upya.

Aidha, alitoa agizo la watumishi wote
wa serikali kurejea kazini ana kwa ana na kuelekeza idara zote kushughulikia mfumuko wa gharama za maisha.

Miongoni mwa maagizo makubwa yaliyosainiwa ni pamoja na kuiondoa Marekani kwenye Mkataba wa Paris wa hali ya hewa, kusitisha utoaji wa fedha kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), na kurejesha Cuba kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi.

Trump pia alisamehe wahalifu wa Januari 6, 2021, akiwemo wale waliopatikana na hatia za njama za uasi.

Kwa upande wa uhamiaji, alitangaza hali ya dharura mpakani, akafuta sera za “Catch and Release” na kutangaza kumaliza uraia wa kuzaliwa kwa watoto wa wazazi wasio raia wa Marekani.

Hatua nyingine ni pamoja na kufuta mipango ya utofauti, usawa, na ujumuishi (DEI) kwenye taasisi za serikali, pamoja na kuondoa haki za kijinsia kwa watu wanaotambua jinsia tofauti na waliyopewa wakati wa kuzaliwa.

Maagizo haya yanatarajiwa kuzua changamoto za kisheria, huku Trump na timu yake wakijipanga kwa kesi nyingi ambazo zinaweza kufunguliwa dhidi ya hatua hizo.

Exit mobile version