Site icon Bongo Plus

Vijana Wameimbishwa Wimbo Wasioujua

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Vijana wengi wa Tanzania hawana uzalendo na hilo Serikali imejifunza na italifanyia kazi huku akisisitiza kuwa Vijana hawajaandamana sababu ya ugumu wa maisha bali ni kwakuwa walilipwa na wengine walifuata mkumbo.

Akiongea na Wazee wa Dar es salaam leo December 02,2025, Rais Samia amesema “Vijana wetu wameingizwa barabarani wakaimbishwa wimbo wasioujua wanadai haki, haki gani!?, mvute Kijana pembeni muulize unadai haki gani!?, na hiyo haki hawakuweza kuidai kwa njia gani hadi waingie njiani wafanye vurugu?, walipwe wakachome vituo?, jingine wanalobebeshwa wameingia njiani eti kwa ugumu wa maisha, Astaghfrullah, ningekuwa na uwezo ningewabeba Vijana wa Tanzania nikawatupe kwenye nchi kadhaa za Afrika pamoja na Majirani zetu wakaone ugumu wa maisha uliokuwepo, halafu waseme kwamba kwao Tanzania ni pahala pema”

“Mwenye ugumu wa maisha kwa raha zake kabisa kweli ataingia njiani akaimbe woyoo woyoo huo ugumu wa maisha?, wenye ugumu wa maisha ataingia kupambana kutafuta chakula, hawa hawakuwa na ugumu wa maisha walikuwa na sababu zao nyingine, Watafiti wafanye utafiti waangalie nafasi ya Tanzania kwenye ugumu wa maisha”

“Vijana wetu wasimezeshwe tu na wenyewe wakameza hapana, haya yanatokea tumejifunza kwamba Vijana wetu wanakuwa tu bila elimu ya uzalendo, Vijana Wazalendo hata upinzani hawakukubaliani na lile, walikuja kutuambia kaeni vizuri wanapanga kufanya hivi, Vijana wetu wengi Tanzania sio Wazalendo na hilo Serikali tumejifunza na tutakwenda kulifanyia kazi”

“Na ndio maana nimeunda Wizara nzima ya Vijana ili kushughulikia Vijana kwa uapana, kwahiyo Vijana wetu hawakuwa na sababu ya msingi ya kuingia barabarani isipokuwa kutumwa na kuingilia mambo yasiyowahusu”

Exit mobile version