Rais wa Marekani Donald Trump amesema amekuwa shabaha kubwa ya kuuawa kutokana na mafanikio ya Uongozi wake, akidai Watu wenye ushawishi mkubwa kama yeye mara nyingi hukumbana na vitisho vya aina hiyo.
Kauli hiyo ameitoa kufuatia tukio la kiusalama lililotokea wakati wa hafla ya Waandishi wa Habari wa Ikulu ya Marekani Mjini Washington.
Tukio hilo ambapo Mtu mwenye silaha alijaribu kuvamia Ukumbi kabla ya kuzuiwa na Vyombo vya Usalama, linaonyesha kwa nini amekuwa akisema mafanikio ya Utawala wake yanamweka kwenye hatari, ambapo katika taharuki hiyo, Maafisa wa Usalama walimtoa haraka yeye pamoja na Wageni wengine muhimu huku akiwataka Wamarekani kubaki na amani licha ya tofauti za kisiasa.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza Trump kukabiliwa na mashambulizi, kwani Julai 13, 2024 alinusurika jaribio la kuuawa wakati wa Kampeni Mjini Butler, Pennsylvania ambapo risasi ilimpiga sikioni, huku Septemba 15, 2024 pia akinusurika tukio jingine la shambulizi karibu na Uwanja wake wa Golf Florida, hivyo tukio hilo jipya la Aprili 2026 linaongeza katika rekodi ya mashambulizi dhidi yake, jambo linaloendelea kuibua mjadala kuhusu usalama wake na athari za kisiasa zinazofuatia.

