Rapa wa Marekani Wiz Khalifa amehukumiwa kifungo cha miezi tisa gerezani nchini Romania baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki dawa za kulevya. Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya Romania zaidi ya mwaka mmoja baada ya tukio lililotokea Julai 2024.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, Wiz Khalifa alikamatwa baada ya kushuhudiwa akitumia bangi jukwaani wakati wa tamasha la Beach, Please! Festival lililofanyika Costineşti. Polisi waligundua kuwa alikuwa na zaidi ya gramu 18 za bangi, jambo ambalo ni kosa la jinai chini ya sheria za Romania.
Mwanzo rapa huyo alipewa adhabu ya faini, lakini upande wa mashtaka uliwasilisha rufaa na mahakama ikaamua kutoa adhabu ya kifungo cha miezi 9, ikisisitiza kuwa sheria za nchi hiyo haziruhusu matumizi au umiliki wa bangi hata kwa matumizi binafsi.
Hadi sasa bado haijawekwa wazi iwapo Wiz Khalifa atalazimika kutumikia kifungo hicho gerezani, au kama kutakuwa na rufaa au makubaliano mengine ya kisheria, ikizingatiwa kuwa ni raia wa Marekani na haishi Romania.
Tukio hili limeibua mjadala mkubwa kimataifa kuhusu tofauti za sheria za dawa za kulevya kati ya nchi mbalimbali, hasa kwa wasanii wanaosafiri na kutumbuiza nje ya nchi zao.

