Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amezindua Benki ya Afrika ya Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu (Africa’s Vegetable Genebank)

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amezindua Benki ya Afrika ya Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu (Africa’s Vegetable Genebank) tarehe 19 Machi 2024, katika Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha.

Benki hiyo inayomilikiwa na Taasisi ya Utafiti na Uendelezaji wa Mazao ya Mbogamboga Duniani (World Vegetable Center – WVC), inakuwa ya kwanza Afrika ikiwa na miundombinu na teknolojia ya kisasa zikiwemo maabara za kisasa zenye uwezo wa kuhifadhi aina 6000 za mbegu tofauti tofauti za mbogamboga kwa takribani miaka 100.

Benki hiyo itarahisisha upatikanaji wa mbegu za mbogamboga kwa wakulima na jamii kwa ujumla na kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora kwa kilimo hicho. Aidha, Benki hiyo pia itarahisisha upatikanaji wa mbegu kwa vizazi vijavyo ikitoa suluhu ya upotevu wa mbegu za mbogamboga inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi Duniani.

Benki hiyo pia itatumika kama kituo cha kufundishia kwa wanasayansi na hata wanafunzi kupitia maabara ya mbegu ambayo ni ya kwanza Afrika, na Tanzania kwa ujumla kupata elimu kuhusu masuala ya mbegu za mbogamboga.

Halfla hiyo imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Emannuela Kaganda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mongella; Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wiebe de Boer; Mwakilishi wa Serikali ya Taiwan Balozi Allen Chenhwa Lou; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Word Vegitable Center Kanda ya Afrika, Dkt. Gabriel Rugalema; ikiwa ni pamoja na viongozi wa Taasisi za Kimataifa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button