Trump aipa Iran nafasi ya mwisho ya mazungumzo, wenyewe wamkazia
Trump aipa Iran nafasi ya mwisho ya mazungumzo, wenyewe wamkazia
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Iran imebakiwa na nafasi moja pekee ya kufikia makubaliano ya amani, kauli inayokuja wakati kukiwa na mkanganyiko kuhusu uwepo wa mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump amedai kuwa Marekani na Iran zimekuwa zikifanya mazungumzo yanayolenga kufikia suluhisho la kumaliza uhasama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo amesema ameahirisha kwa muda wa siku tano mashambulizi aliyokuwa ametishia kuyafanya dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran, akieleza kuwa anatoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia.
Hata hivyo, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad-Bagher Ghalibaf amesema hakuna mazungumzo yaliyofanyika kati ya nchi hiyo na Marekani, akisema taarifa hizo kuwa ni habari za uongo na zenye lengo la kupotosha na kuathiri mwenendo wa soko la mafuta duniani.
Pamoja na msimamo huo, taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran zinaeleza kuwa nchi hiyo imepokea mapendekezo kutoka Marekani kupitia wapatanishi.





