Wadukuzi Iran Wadukua Email ya FBI
Wadukuzi Iran Wadukua Email ya FBI
Wadukuzi wanaodaiwa kuhusishwa na Serikali ya Iran wamefanikiwa kudukua akaunti binafsi ya barua pepe ya Mkurugenzi wa Ofisi ya Upelelezi ya Shirikisho la Marekani, (FBI), Kash Patel, na kuanika sehemu ya taarifa walizozipata mtandaoni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Shirika la Habari la CNN pamoja na chanzo kilicho karibu na tukio hilo, Wadukuzi hao walichukua nyaraka, picha na mawasiliano mbalimbali ya zamani ya Patel kabla hajateuliwa kuongoza FBI na baadhi ya nyaraka hizo zimethibitishwa kuwa halisi.
Inaelezwa kuwa barua pepe zilizodukuliwa zinahusiana na kipindi cha kati ya mwaka 2011 hadi 2022, zikijumuisha mawasiliano binafsi, shughuli za kibiashara pamoja na safari zake za kikazi na binafsi katika kipindi hicho.
Hata hivyo, Mtaalamu wa Usalama wa Mtandao kutoka Marekani, Ron Fabela, amesisitiza kuwa tukio hilo halihusiani na kuvamiwa kwa mifumo rasmi au ya siri ya FBI, bali ni udukuzi wa akaunti binafsi ya barua pepe ambayo haikuwa sehemu ya miundombinu ya Serikali.
Kwa upande wake, FBI imethibitisha tukio hilo na kusisitiza kuwa hakuna taarifa nyeti za serikali zilizovuja. Aidha, taasisi hiyo imetangaza zawadi ya dola milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kubaini kundi la Wadukuzi linalojiita “Handala Hack Team” ili wachukuliwe hatua za kisheria.





