Boti yakamatwa ikiwa na shehena ya mirungi Bagamoyo
Boti yakamatwa ikiwa na shehena ya mirungi Bagamoyo
Siku moja baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kueleza kwamba imebaini ongezeko la uingiaji na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, shehena nyingine ya dawa hizo imekamatwa ikiwa inaingizwa nchini kutokea Mombasa nchini Kenya.
Dawa hizo zilizokuwa zimefungashwa kwenye vifurushi 1,062 na kuwekwa kwenye viroba 18 zilikamatwa kwenye boti ya kisasa katika ufukwe wa Magambani eneo la Kaole Ufundi Bagamoyo.
Sambamba na dawa hizo wamekamatwa pia watuhumiwa wanne ambao wote ni raia wa Tanzania, wawili wakiwa wakazi wa Tanga na wengine wawili wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Hili linakuja baada ya DCEA kubaini kukua kwa mtandao wa biashara ya mirungi na kusababisha uingizaji wa dawa hizo kuongezeka nchini ambapo kwa Machi pekee kilogramu 1267.12 zilikamatwa.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kukamatwa kwa boti hiyo usiku wa kuamkia Aprili 14, 2026 matokeo ya operesheni iliyofanyika kuubaini mtandao wa biashara ya mirungi nchini ambayo inaonekana kushika kasi siku za karibuni.
Amesema baada ya kazi kubwa kufanyika katika kutokomeza dawa za kulevya za viwandani na bangi, sasa hivi matumizi yameongezeka kwa kasi kwenye mirungi hivyo mbinu mbalimbali zinafanyika kuingiza dawa hizo nchini.
Lyimo amesema operesheni hiyo ilifanyika baada ya kupatikana kwa taarifa kuhusu uwepo wa mtandao unaojihusisha na uingizaji wa dawa hizo kupitia njia za majini.






