Watatu wafariki dunia mlipuko wa ugonjwa ‘hantavirus’ wakiwa safarini
Watatu wafariki dunia mlipuko wa ugonjwa 'hantavirus' wakiwa safarini
Watu watatu wameripotiwa kufariki dunia kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya hantavirus katika meli ya kitalii iliyokuwa safarini kutoka Argentina kuelekea Cape Verde, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Taarifa zinaeleza kuwa, mwanamume mwenye umri wa miaka 70 alipatwa na dalili za ugonjwa huo akiwa ndani ya meli ya MV Hondius huku mkewe, ambaye pia alipata dalili za ugonjwa huo, alifariki dunia akiwa amelazwa hospitalini jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Wawili hao walikuwa raia wa Uholanzi.
Aidha, chanzo kinaelezwa kuwa mgonjwa wa hantavirus raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 69 ambaye kwa sasa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) jijini Johannesburg, akiwa katika hali mbaya.
Katika tukio hilo, wahudumu wawili wa meli hiyo pia wameripotiwa kuwekwa chini uangalizi wa matibabu baada ya kuonesha dalili zinazofanana na maambukizi hayo.
Maofisa wa Uholanzi wameeleza kuwa wanapanga kuwarejesha nchini humo watu wawili wenye dalili pamoja na miili ya marehemu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, virusi vya hantavirus husambazwa na panya, hasa kupitia hewa yenye chembechembe kutoka kinyesi au mkojo wa panya. Hata hivyo, maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda mwingine ni nadra sana kutokea.





