Iran Yamjibu Trump: Hormuz Haitoendeshwa na Post Zake Kidanganyifu
Iran Yamjibu Trump Hormuz Haitoendeshwa na Post Zake
Mvutano kati ya Iran na Marekani umechukua sura mpya baada ya viongozi wa Iran kumjibu vikali Rais wa Marekani Donald Trump, wakisema Mlango wa Hormuz “hautatawaliwa na machapisho yake ya kidanganyifu.”
Kauli hiyo imetolewa na afisa wa juu wa bunge la Iran, Ebrahim Azizi, kufuatia mpango wa Marekani (Project Freedom) wa kuingilia usafirishaji wa meli katika eneo hilo.
Iran imeonya siku ya leo kuwa hatua yoyote ya Marekani kuingilia Mlango wa Hormuz hasa kupitia operesheni ya kusindikiza meli itachukuliwa kama ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, na inaweza kusababisha kurejea kwa mapigano makubwa.
Mvutano huu unakuja wakati ambapo Marekani imezindua mpango wa kusaidia meli zilizokwama katika njia hiyo muhimu ya kimataifa, huku Iran ikisisitiza kuwa udhibiti wa Hormuz uko mikononi mwake na haitakubali kuingiliwa na nguvu za kigeni.
Kwa upande mwingine, taarifa za kimataifa zinaonesha kuwa hali katika Mlango wa Hormuz bado ni tete, huku pande zote zikiongeza presha ya kijeshi na kidiplomasia, jambo linaloifanya dunia kuendelea kufuatilia kwa karibu iwapo mgogoro huu utaishia kwenye mazungumzo au vita kamili kwa mara nyingine tena.





