WAZIRI MKUU: TANZANIA IKO SALAMA DHIDI YA EBOLA*
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania inaendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa wa Ebola huku Serikali ikiendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari, ufuatiliaji na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa ya mlipuko.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 4, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asha Salum Moto, ambaye alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na ugonjwa wa Ebola unaoripotiwa katika baadhi ya nchi jirani.
“Mpaka sasa tuko salama, nchi yetu iko salama. Ni jambo la kumshukuru Mungu. Hata hivyo, kwa kuwa Tanzania si kisiwa, tunaendelea kuchukua hatua zote za tahadhari ili kuhakikisha usalama wa wananchi wetu unaendelea kuwepo,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, kuimarisha ufuatiliaji mipakani pamoja na kuhimiza utoaji wa taarifa mapema pale dalili za magonjwa hayo zinapojitokeza.
“Tuendelee kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya na tusifiche dalili wala taarifa zinazoweza kusaidia kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko,” amesema.
Katika swali jingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya reli na miundombinu mingine ya usafiri ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na ukuaji wa miji na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Haran Sanga, ambaye alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya reli katika majiji yanayokuwa kwa kasi nchini.
“Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za mzunguko katika miji mikubwa na kukamilisha miradi ya reli ya kimkakati. Kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu, tutaendelea kuwekeza pia katika reli za ndani ya majiji yetu,” amesema.






