CRDB Bank Yadhamini Manyara Tanzanite Marathon 2026 Kuboresha Huduma za Afya Hanang

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa CRDB Bank ambapo benki hiyo kupitia bidhaa yake ya Imbeju imethibitisha kuwa mdhamini mkuu wa mbio za hisani za Manyara Tanzanite Marathon 2026 zitakazofanyika tarehe 22 Agosti mjini Babati.

Marathon hiyo inalenga kuchangia uboreshaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang, hususan kwa watoto wachanga na watoto njiti kupitia upatikanaji wa vifaa tiba muhimu, ikiwemo incubator na mahitaji mengine yatakayosaidia kuokoa maisha ya watoto.

Mhe. Sendiga ameushukuru uongozi wa CRDB Bank kwa kuunga mkono dhamira hiyo yenye kauli mbiu ya *“Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto”*, akieleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara.

Tukio hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, likiwa na lengo la kuhamasisha mshikamano katika kuokoa maisha ya watoto na kuboresha huduma za afya.

Mkoa wa Manyara unaendelea na maandalizi ya kuhakikisha Manyara Tanzanite Marathon 2026 inakuwa tukio la kihistoria lenye manufaa makubwa kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button