Ndege ya Jeshi Yauwa 8 Marekani
Ndege ya Jeshi Yauwa 8 Marekani
Ndege ya Kijeshi ya Marekani aina ya B-52 Stratofortress imeanguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards kilichopo katika Jangwa la Mojave, Kusini mwa Jimbo la California.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Maafisa wa Kituo hicho cha Jeshi, Watu wote wanane waliokuwa ndani ya ndege hiyo wanahofiwa kufariki dunia baada ya ajali hiyo.
Ndege hiyo ya Boeing yenye injini nane, ambayo hutumika kubeba mabomu ya Nyuklia na mabomu ya kawaida, ilikuwa katika safari ya kawaida ya majaribio wakati ilipoanguka.
Picha za video zilizorekodiwa kutoka angani zimeonesha eneo kubwa la jangwa lililoungua na kuendelea kutoa moshi, lenye ukubwa unaokadiriwa kufanana na Uwanja wa Mpira wa miguu. Magari ya huduma za dharura yalionekana yakifanya operesheni katika eneo la tukio.
Ajali hiyo imetokea usiku wa Juni 15 ikiwa ni takribani kilomita 161 Kaskazini mwa Jiji la Los Angeles, huku uchunguzi ukitarajiwa kuanza kubaini chanzo cha tukio hilo.





