Mtoto mbaroni akituhumiwa kumuua baba yake Dar, afukia mwili chumbani
Mtoto mbaroni akituhumiwa kumuua baba yake Dar, afukia mwili chumbani
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imemtia mbaroni Juma Ramadan (21), maarufu Juli, mkazi wa Ubungo, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Ramadan Jafar (47), maarufu Muna, ambaye awali aliripotiwa kupotea.
Kwa mujibu wa polisi, baada ya kudaiwa kufanya mauaji hayo, polisi ilieleza kuwa mtuhumiwa alichimba shimo ndani ya moja ya vyumba vya nyumba hiyo na kuufukia mwili wa baba yake, ambaye kabla ya kifo chake alikuwa akitumia chumba hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Jumanne, Juni 23, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema Juni 16, 2026, Kituo cha Polisi Kimara Gogoni kilipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Ramadan Jafar kuhusu kupotea kwake.
Amesema uchunguzi huo ulibaini mtu aliyeripotiwa kupotea alikuwa ameuawa na mwili wake kufukiwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumba yake iliyopo Mbezi Luguruni Kwembe, Wilaya ya Ubungo.
“Uchunguzi wa awali ulionyesha mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa mtoto wa marehemu, ambaye naye alikuwa ametoweka baada ya tukio hilo,” amesema Muliro.





