Wadau wa maendeleo katika sekta ya afya waipongeza Tanzania kwa kuanzisha mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii
Wadau wa maendeleo katika sekta ya afya waipongeza Tanzania kwa kuanzisha mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii utakaowafikishia wananchi huduma za kinga, tiba na elimu ya afya mahali walipo bila vikwazo vyovyote.
Wadau hao wameipongeza Tanzania baada ya Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu kuwaeleza umuhimu wa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) ikiwa ni mkakati wa kuimarisha utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi na kufikia lengo la afya kwa wote.
Waziri Ummy amesema hayo kwenye mkutano uliofanyika pembezoni mwa mkutano mkuu wa 77 wa shirika la afya duniani (WHO), unaoendelea Jijini Geneva nchini Uswisi uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Mkutano huo ambao umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika na mabara mengine, umedhihirisha wazi matarajio na mategemeo ya wadau kuwa mpango huo utakuwa wa mfano katika kuboresha uratibu wa afua mbalimbali za Afya zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.







