Raisi Mnangawa akabidhi eneo la ujenzi wa makumbusho ya ukombozi wa Afrika
Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa leo tarehe 8 Agosti, 2024 jijini Harare amezindua ujenzi wa Makumbusho ya Urithi wa Afrika na kukabidhi eneo la hekta moja (1) kwa ajili ya uhifadhi wa historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika linalotambulika kama Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC au “SADC Liberation Square”.
Mhe. Mnangagwa alikabidhi Kituo hicho rasmi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, ambapo kilipokelewa kwa niaba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi na kueleza kuwa Kituo hiko kitachangia juhudi za Kanda za kuenzi michango ya Wapigania uhuru katika harakati za ukombozi na pia ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kuenzi Waanzilishi wa SADC.








