Ndege Yaangukia Makazi, Yaua Watu Wawili.

Ndege Yaangukia Makazi Yaua Watu Wawili

Watu wawili waliokuwa ndani ya Ndege ndogo aina ya Piper PA-28 wamefariki dunia baada ya Ndege hiyo kuanguka kwenye Nyumba katika Mji wa Akron, Jimbo la Ohio Nchini Marekani, huku Idara ya Zimamoto ya Akron ikithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Ndege hiyo iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Akron Fulton uliopo takribani maili nne kutoka eneo la tukio kabla ya kuanguka Alhamisi Mei 14, 2026 na kusababisha mlipuko mkubwa wa moto baada ya kugonga Nyumba iliyopo katika eneo la makazi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, Watu wote waliokuwa ndani ya Ndege hiyo wamefariki papo hapo, kukiwa hakuna majeruhi walioripotiwa kwa Wakazi wa Nyumba iliyogongwa, ingawa Wakazi wa Nyumba hiyo pamoja na majirani wa maeneo ya karibu wamehamishwa kwa tahadhari kutokana na moto mkubwa na moshi mzito uliotanda eneo hilo.

Mkuu wa Idara ya Zimamoto ya Akron, Sierjie Lash, amesema wamepokea simu nyingi kutoka kwa Wananchi waliokuwa wakiripoti kusikia milipuko kabla ya Vikosi vya Zimamoto kufika eneo la tukio na kukuta Nyumba ikiwa imeteketea kwa moto mkubwa.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) pamoja na Bodi ya Taifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) zimeanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku majina ya Watu waliopoteza maisha bado hayajatolewa rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button