Wasusia Msiba Wakitaka Mfiwa Aombe Msamaha.
Wasusia Msiba Wakitaka Mfiwa Aombe Msamaha
Wakazi wa Mtaa wa Kambarage katika Halmashauri ya Mji wa Njombe wamesusia mazishi ya Mwananchi Mkazi wa eneo hilo kwa madai kuwa mfiwa ambaye ni Mke wa marehemu alikuwa hashiriki shughuli za misiba pamoja na kutotoa michango mbalimbali ya Kijamii inayohitajika katika Mtaa huo.
Sintofahamu hiyo imetokea Mei 14, 2026 katika eneo la Block X, ambapo baadhi ya Waombolezaji akiwemo Ester Mtweve wamesema ushiriki katika shughuli za Kijamii ni muhimu kwa kudumisha mshikamano na kusaidiana wakati wa matatizo, lakini mfiwa huyo alikuwa haoni umuhimu wa kushiriki.
“Mfiwa alikuwa hajumuiki kwenye shida za wenzake na Watoto anawafungia ndani, leo Mwanaume yuko Mochwari na maiti inaenda kuchukuliwa na Ndugu upande mmoja,” amesema Ester.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambarage, Fransis Msanga, ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kushiriki katika matukio mbalimbali ya Kijamii ikiwemo misiba pamoja na kuchangia michango inayotangazwa kwa mujibu wa utaratibu wa Mtaa, huku akiwataka Wananchi kuona umuhimu wa kudumisha upendo, umoja na ushirikiano bila kujali tofauti zilizopo.
Hata hivyo, baada ya mvutano wa muda mrefu, mfiwa Beatha Mgaya amelazimika kuwaomba radhi Wananchi ndipo Waombolezaji wakaridhia kushiriki mazishi hayo.





