Serikali ya Tanzania na India zimekubaliana kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey, aliyefika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha. jijini Dar es Salaam kujitambulisha.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa katika kipindi ambacho Tanzania inatekeleza Dira ya Taifa 2050, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya India, wakati ambapo uhusiano wa kidiplomasia, kijamii na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuimarika.

Alieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umejengwa katika misingi imara ya ushirikiano wa muda mrefu, uliowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta za maji na afya, yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

“Uhusiano wetu ni wa muda mrefu na umeanza hata kabla ya kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia ambapo watu kutoka pande hizi mbili walikuwa wakisafiri na kufanya biashara kupitia Bahari ya Hindi, na leo hii ushirikiano wetu umejikita katika nyanja za kibalozi, kiuchumi na kijamii,” alisema Balozi Omar.

Akizungumzia sekta ya maji, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia ushirikiano na India, huku changamoto zilizojitokeza zikishughulikiwa kwa kushauriana na kushirikiana kwa karibu kati ya nchi hizo mbili.

Katika sekta ya elimu, Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa India imeanzisha chuo Zanzibar kinachotoa mafunzo ya Sayansi ya Data na Akili Unde (AI), pamoja na kozi za muda mfupi na mrefu.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo si tu inanufaisha Watanzania, bali pia wanafunzi kutoka mataifa mengine ya Afrika, hivyo kutoa fursa muhimu ya kukuza ujuzi na teknolojia barani humo.

Aidha, alieleza kuwa India imeendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania, hususan katika sekta ya afya, ambapo wataalamu wengi wamepata mafunzo nchini humo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button