Waziri Mkuu wa Ethiopia anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 29 Februari hadi 02 Machi, 2024 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Lengo la ziara hii mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia ambazo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama.

Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie. Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa Viongozi Waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button