Ujenzi Wa Daraja La Magufuli Mbioni Kukamilika Mita 2
Ujenzi Wa Daraja La Magufuli Mbioni Kukamilika Mita 2

Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo- Busisi) lenye urefu wa kilometa tatu linalojengwa kuunganisha barabara kuu ya Usagara Sengerema – Geita katika Ziwa Victoria, lipo mbioni kukamilika, kwani kimebaki kipande cha mita mbili kuunganishwa.
Hayo yameelezwa jana Jumanne Septemba 17, 2024 mkoani Mwanza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alipokagua ujenzi wa daraja hilo unaoenda sambamba na ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 upande wa Kigongo na Busisi.
“Nimetembea kilometa tatu za Daraja la J.P Magufuli kujionea kazi, nimejiridhisha tumebakiza mita mbili ndicho kipande kilichobaki kukamilisha ujenzi wa kilometa tatu za daraja hili pamoja na barabara za maungio kiliometa 1.66 ambazo pia ujenzi unaendelea, amesema Bashungwa.
Bashungwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kuendeleza miradi yote iliyoasisiwa na hayati John Magufuli kwa kuendelea kutoa fedha, ili ujenzi wa daraja ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha mkandarasi analipwa malipo yake, hivi karibuni amepokea Sh18 bilioni zitakazomuwezesha kukamilisha ujenzi wadaraja hilo ifikapo Desemba 2024.
Aidha, Bashungwa amempongeza Meneja wa Wakala ya Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, mhandisi mshauri kampuni ya Yooshin Engineering Corporation (Korea) na mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Bashungwa ameeleza ujenzi wa daraja hilo umetoa fursa kwa wataalamu wa ndani na wahitimu wa kada ya ujenzi kupata ujuzi na uzoefu, utakaosaidia kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, mhandisi mshauri wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, Abdulkarim Majuto ameeleza ujenzi daraja hilo umefikia asilimia 90.5 na kazi zinaendelea kufanyika usiku na mchana na kwamba matarajio hadi kufikia mwanzoni mwa Oktoba 2024, daraja hilo liwe limeunganishwa.









