Marekani – Abiria 179 wa shirika la ndege la Marekani Denver Airlines wamenusurika kifo baada ya ndege waliokuwa wakisafiria kushika moto

Abiria 179 wa shirika la ndege la American Airlines wamenusurika kifo baada ya ndege waliokuwa wakisafiria kushika moto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Denver, muda mfupi kabla ya kuondoka kuelekea Miami.

Tukio hilo lilitokea wakati ndege aina ya Boeing 737 MAX 8, nambari ya safari AA 3023, ikiwa tayari kwenye njia ya kurukia ndege.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka za usalama, moto ulianzia kwenye sehemu ya magurudumu ya nyuma upande wa kushoto wa ndege, na kusababisha rubani kusitisha safari mara moja.

Moto huo uliosababisha moshi mzito uliwalazimu wahudumu wa ndege kuamuru abiria kutumia milango ya dharura na kushuka kwa kutumia mabembea ya dharura.

Video zilizosambaa mitandaoni zinaonesha abiria wakikimbia kwa hofu huku moshi mzito ukitanda kwenye eneo la tukio.

Taarifa za awali kutoka kwa maafisa wa zimamoto na uokoaji zinaeleza kuwa mtu mmoja alipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, huku wengine wakipata huduma ya kwanza katika uwanja wa ndege kutokana na majeraha madogo na mshtuko wa tukio hilo.

Shirika la Federal Aviation Administration (FAA) limethibitisha kuwa limeanzisha uchunguzi rasmi wa tukio hilo, huku ndege husika ikiondolewa kwenye huduma kwa ajili ya uchunguzi wa kiufundi.

Hili linakuwa tukio la pili mwaka huu katika uwanja huo huo likihusisha shirika la American Airlines. Mnamo Machi 2025, ndege nyingine ya shirika hilo iliungua moto baada ya kutua kwa dharura, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.

Mamlaka zimewahakikishia wasafiri kuwa hatua madhubuti zinachukuliwa kuhakikisha usalama wa safari za anga unaimarishwa

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button