Aliyepinga Raila Odinga Kuzikwa Ndani ya Saa 72 Akwama Mahakamani.
Aliyepinga Raila Odinga Kuzikwa Ndani ya saa 72 Akwama Mahakamani
Mahakama Kuu nchini Kenya imekataa ombi la kusitisha agizo la kuzikwa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga, ndani ya saa 72, ikisema mleta maombi hakuonyesha uhitaji wa dharura wa kuingilia kati mchakato wa mazishi hayo.
Jaji Chacha Mwita ametoa uamuzi huo jana, Alhamisi, Oktoba 16, 2025, akibainisha kuwa mlalamikaji hakuweza kuthibitisha kama maandalizi ya mazishi yalikuwa yakifanywa kinyume na matakwa ya marehemu.
“Baada ya kuzingatia maombi hayo, sijaridhishwa na uhitaji wa suala hili. Mshitaki hajaonyesha kuwa mchakato wa maziko unafanyika kinyume na matakwa ya marehemu, jambo ambalo lingehalalisha mahakama hii kutoa amri ya kusitisha shughuli hizo,” amesema Jaji Mwita.
Uamuzi huo unafuatia ombi lililowasilishwa na Michael Onyango Otieno, aliyedai kuwa kuharakishwa kwa mazishi ya Odinga ndani ya saa 72 kunakiuka Katiba ya Kenya, hasa Kifungu cha 44, kinachohakikisha haki ya kila mtu kushiriki katika maisha ya kitamaduni ya jumuiya yao.
Otieno alitaka mahakama itamke kuwa utaratibu huo wa maziko unakiuka haki za wananchi wanaotaka kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa upinzani aliyekuwa na mchango mkubwa katika siasa za nchi hiyo.





