Chris Brown Achukia Kulinganishwa na Wasanii Wengine
Chris Brown Achukua Kulinganishwa na Wasanii Wengine
Msanii nyota wa R&B, Chris Brown, ameibua hisia kali Jumamosi hii kupitia Insta Story yake baada ya kile alichokieleza kama kero ya muda mrefu ya kulinganishwa na wasanii wengine bila sababu ya msingi.
Katika ujumbe wake uliosambaa kwa kasi mitandaoni, Breezy aliandika:
“Natamani muache kunilinganisha na wasanii wengine na kusema ni mimi dhidi ya fulani. Mpaka msanii mmoja kati ya hao afanye mambo haya yote peke yake bila msaada wowote huku vyombo vya habari vikiendelea kuniharibia kila mara, ndipo mje mniambie.”

Chris Brown aliweka bayana kuwa hana muda wa kushindana na yeyote na kwamba yeye hulenga kuwahudumia mashabiki zake wa kweli kupitia jukwaa lake la Breezy Bowl, ambalo alisema ni kwa wale “wanaotaka kuwepo kwa dhati.”
Akiendelea kwa maneno ya uchungu, aliongeza:
“Najaribu kuilisha familia yangu! Sina muda na msanii mwingine wala ninachojali wanachofanya!”
Brown pia alilalamikia kutotambuliwa licha ya kujitolea kwake katika tasnia:
“Nimekuwa nikijituma kupita kiasi kwa miaka 20 iliyopita, na najua sitawahi kutambuliwa kwa chochote zaidi ya drama!
Kwahiyo niepusheni na maneno yote hayo tafadhali!”
Ujumbe huu unakuja wakati ambapo mashabiki na vyombo vya habari mara kwa mara hujaribu kumlinganisha Chris Brown na wasanii wengine, huku wengi wakichanganya mafanikio ya kisanii na maisha ya kibinafsi yenye utata.





