Dkt Mwinyi-Ufunguzi wa uwanja wa kisasa wa michezo Kitope leo tarehe 09 Septemba 2025,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Awamu ya Nane imejipanga kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya michezo kwa kujenga viwanja vya kisasa ili kuibua vipaji na kukuza wataalamu wa soka. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa uwanja wa kisasa wa michezo Kitope leo tarehe 09 Septemba 2025, Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa hatua za awali tayari zimevuka malengo ya Ilani ya CCM 2020–2025 kupitia ujenzi wa viwanja vya mikoa na wilaya.
Ameeleza kuwa Zanzibar imebahatika kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya CHAN yaliyomalizika hivi karibuni, pamoja na AFCON 2027, ambayo yanahitaji maandalizi ya kiwango cha juu. Aidha, Serikali imekamilisha ukarabati wa viwanja vya New Amani Complex, Mao Tse Tung na Gombani, sambamba na kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanja vipya vya Kizimkazi na Fumba, pamoja na viwanja 17 vya mikoa na wilaya Unguja na Pemba.
Dkt. Mwinyi amesema lengo ni kuhakikisha kila kipaji kinaonekana, kinakuzwa na kuendelezwa, huku michezo ikitumika kama nyenzo ya burudani, urithi wa utamaduni, kukuza utalii na kutoa ajira kwa vijana. Ameongeza kuwa viwanja vipya vitapunguza changamoto zinazowakabili vijana, wanawake na makundi yenye mahitaji maalumu, na kuifanya michezo kuwa jumuishi na chachu ya amani na mshikamano wa kitaifa.






